“Siwezi kufanya hivi tena. Siwezi kuwa na wewe bila
kukuona kwa namna ninavyotaka mimi. Shauku ya wewe kuwa wangu inazidi maadili
yangu, inazidi uwezo wangu wa matamanio. Siwezi tena kujifanya kama sioni jinsi
gani nikiangalia macho yako na kujidanganya kwamba… chochote tulicho nacho…
kinaenda kwa jinsi unavyotaka.”
“Sijui nifanye nini ili uhisi ninavyohisi mimi. Labda
huwezi kuona hili, lakini angalau jaribu kunitaka kama ninavyokutaka mimi,
tumegawana hisia zetu, matatizo yetu, miili yetu. Kwanini iwe vigumu kuukubali
uhalisia wa mahusiano yetu?”
“Unanipenda?”
Swali hilo. Swali ambalo hutaki kulisikia masikioni
mwako. Swali ambalo huna jibu nalo. Kutarajia jibu kutoka kwa mtu usiyemtaka
kumpoteza ni kama kisu kichanjacho moyoni. Ninajua hilo, kujua kwamba jibu
litakalotoka litauma hata kama watabaki au kuondoka. Unatazama macho yake
yaliyojaa hasira, ukihisi njaa iliyoko kwenye mtazamo wake. Maneno yanakukwama
kooni na kushindwa kuongea. Unashusha macho, ukitamani aseme chochote ili kuvunja
ukimya.
Anaangalia kando, na kuelekea mlangoni. Lakini anasita
kabla ya kutoka chumbani. Unatamani kusema chochote kumbembeleza abaki, upande
mwingine unatamani aende umruhusu awe huru na hisia zake ili pia kuulinda ukuta
ulioujenga moyoni mwako.
“Siwezi kufanya hivi tena. Kwaheri.”
Anatoka akikuacha umesimama pale pale bila kujua cha
kufanya. Mwili wako unapwaa baridi, mikono yako imejifunga kifuani kwa nguvu
huku hisia za upweke zikipenya ndani yako na kukukamata kabisa. Unapumua
polepole, macho yako yakielekeza mboni zake mlangoni, mlango ambao umeshuhudia
akiufungua na kuondoka. Unajaribu kuelewa na kukubaliana na uhalisia wa upweke
ulionao, lakini upweke huo inakuzidi nguvu na kujifanya ujikaze kwa kila nguvu
uliyonayo.
Muda unasonga mbele, lakini bado umekwama palepale
kwenye wakati ulioachwa na uhalisia mgeni. Huwezi kusonga mbele hata kama
ukijitahidi kutumia nguvu zako zote. Wakati ambao neno lako moja lingebadili
kila kitu hukulisema. Na sasa, majuto yanakutafuna kama njaa isiyoshiba. Maisha
yako yamekuwa mzunguko usio na hisia, kuamka, kula, kufanya kazi na kulala,
kama mashine ya kiotomatiki. Unajipa mawazo kuwa umefamya maamuzi sahihi,
uamuzi uliotokana na kujilinda na kuhifadhi moyo wako. Lakini ule uchungu usiokomaa
ndani ya kifua chako, unakusaliti, unakuwa sauti ya daima inayokukumbusha maamuzi
yako.
Unachukua simu na kuanza kupitia mitandao ya ya
kijamii, kidole gumba chako kinakosa nguvu, ukitafuta dalili yoyote ya wewe
kuwepo kati ya misururu isiyoisha ya machapisho. Hakuna kitu kipya. Chapisho
lake la mwisho ni picha yenu wawili, mikono yake ikiwa imezunguka kiuno chako,
mkono wako ukiwa begani mwake, nyote wawili mkiwa kwenye tabasamu zito.
Unakazia macho picha hiyo, ukikumbuka furaha uliyowahi kuihisi, ingawa uchungu
bado upo ndani kabisa ya moyo yako, tabasamu laini linajitokeza bila hiari
kwenye midomo yako.
Unazima simu yako na kutoka nje. Kumbukumbu ya jinsi
mlivyokutana kwa mara ya kwanza inakurudia, siku zako za chuo kikuu., kozi
tofauti mlizosoma watu mbali mbali mliokutana nao, na urafiki wa haraka lakini
wenye kina mliouanzisha.
Uliwahi kuzungumzia ndoto zako kwa uwazi, ulilia kwa
kicheko, ulikabiliana na maumivu kwa ujasiri. Lakini cha kushangaza, haujawahi
kushawishika kuhusu uwezekano wa mapenzi. Kwako, mapenzi yalikuwa mtego,
kujisalimisha kwa uhuru, gereza lililojengwa kwa petali za waridi na miiba.
Maumivu ya zamani yalikuongoza kuapa kuwa hutamruhusu mtu yeyote adhibiti moyo
wako tena.
Alijua. Alijua kuwa hutaki kwenda mbali zaidi kwenye
mahusiano yenu. Lakini aliacha mapenzi yachukue nafsi yake kama mzizi laini ya
maumivu matamu na machungu. Unakumbuka usiku ambao kila kitu kilibadilika baina
yenu. Mchezo wa ukweli na kuthubutu ulisababisha busu mwanana lililozidisha
matamanio ya mwili kati yenu. Busu hilo likazua muunganiko ambao usingeweza
kupuuza. Kuta ulizojenga kulinda urafiki wenu zilibomoka chini ya uzito wa
tamaa mliyoshiriki.
Hata hivyo, uliweka sheria mpya kwenye uhusiano wenu,
ukauita urafiki wa kufaidiana. Bila ahadi wala matarajio ya uhusiano wa
kimapenzi wa kudumu, bila hisia, miili tu ikijikunyata pamoja. Aliyakubali
masharti yako, ingawa ulikuwa unaona upendo wake ukititrika usoni mwake, ila
ulivaa upofu ukijifanya huoni chochote. Macho yake yalikaa juu yako muda wowote
akuangaliapo, mguso wake ulikuwa mpole na alioyesha kutaka zaidi lakini
aliogopa kuvuka mipaka ya masharti yako.
Sasa umekaa peke yako, mzigo wa maamuzi yako
ukikuelemea. Unatazama taswira yako kwenye kioo. “Lazima niweke sheria
nyingine,” unanong’ona. “Nitajutia baadaye.”
Unachukua simu yako na kuelekea nyumbani kwake. Moyo
wako unadunda kwa nguvu kadri unavyokaribia mlango wake. Je, umechelewa? Huenda
hisia zake zimefifia? Je, kama tayari amesonga mbele?
Unasita kwa
muda mchache na kisha kusukuma mlango kwa pupa, huwezi kuzuia hisia zako tena.
“Vera?” Sauti yake ni laini, yenye mshangao.
“Sielewi kinachonikuta,” unasema kwa haraka,
ukizunguka ndani ya chumba. “Najihisi kama napoteza akili. Tumbo linavurugika,
kichwa changu ni kama kimechanganyikiwa, umejaa wewe tu. Natamani nikutoe
akilini mwangu lakini inashindikana.”
“Vera, kuna nini?”
“kuna nini kati yetu?” unauliza kwa sauti kali “Huwezi
tu kuondoka kama unavyotaka unajua ni jinsi gani ninavyokuhitaji. Moyo unauma,
Max. inauma kukupoteza.”
Chumba kinatulia. Unahisi joto likipanda mashavuni
mwako baada ya mlipuko wako wa hisia, na kwa aibu, unageuza macho yako pembeni,
ukizidiwa na hisia za aibu na majuto.
“Vera,” anakuita kwa sauti ya chini, “Unaingia kwenye
upendo, sio ugonjwa wala sio jambo baya.”
“Ninakuchukia,” unakiri, machozi yakikutoka.
Anapiga magoti mbele yako, akishika mikono yako
miwili. “Basi nichukie kwa kukupenda. Nichukie kwa kutaka zaidi kutoka kwako.
Lakini usinisukume mbali na uwepo wako.”
“Max,”
Anatabasamu, “Kama itakufanya uhisi afadhali unaweza
kusema ‘nakuchukia” kadri uwezavyo badala ya ‘nakupenda”
“Nakuchukia,” unanong’onoa kwa sauti ya chini ukitoa
tabasamu la mbali.
“Inakusaidia?”
“Kidogo,” Unasema, ukimvuta karibu zaidi.
Busu lake ni la taratibu na lenye upole. Akikubusu,
mikono yake anazungusha kiunoni mwako na kukuleta zaidi mwilini mwake bila
kuacha nafasi yoyote baina yenu. Kadri akikubusu kuta ulizojenga kuzunguka moyo
wako zinabomoka taratibu zikiacha hisia zako bila kinga. Safari hii, unafanya
uamuzi wa makusudi kuziacha zianguke chini kabisa...
Comments
Post a Comment